Kenya Certificate of Secondary Education Kiswahili – Fasihi Karatasi ya 3

SEHEMU A: RIWAYA

A. Matei: Chozi la Heri

1. Lazima

(a) “Sasa haya ameyapa kisogo … kufunguliwa kwa kituo hiki ni kama mana iliyomdondokea kinywani kutoka mbinguni.”

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(ii) Bainisha tamathali mbili za usemi ambazo zimetumiwa katika dondoo hili. (alama 2)

(iii) Fafanua umuhimu wa mhusika anayerejelewa katika dondoo hili katika kuijenga riwaya hii. (alama 6)

(b) Jadili mikakati mwafaka ambayo vijana wanatumia kukabiliana na hali yao ya maisha kwa kuwarejelea wahusika wafuatao:

(i) Chandachema (alama 4)

(ii) Dick (alama 4)

SEBEMU B: TAMTHILIA

P. Kea: Kigogo

Jibu swali la 2 au la 3

2. (a) Jadili mbinu kumi ambazo Wanasagamoyo wanatumia kupigana na utawala dhalimu. (alama 10)

(b) Eleza jinsi mbinu rejeshi ilivyotumiwa kukuza vipengele vifuatavyo katika tamthilia hii.

(i) Maudhui (alama 5)

(ii) Wahusika (alama 5)

3. (a) “Ushahidi utatoka wapi kama kipanga ndiye hakimu kwenye kesi ya kuku?”

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)

(ii) Fafanua dhima ya vipengele viwili vya kimtindo vinavyobainika katika dondoo hili. (alama 4)

(b) (i) Kwa kurejelea tamthilia jadili sifa sita za msemaji.(alama 6)

(ii) Eleza umuhimu wa mandhari katika tamthilia hii. (alama 6)

SEHEMU C: HADITHI FUPI

Jibu swali la 4 au la 5

A. Chokocho na D. Kayanda (Wah): Tumbo Lisiloshiha na Hadithi Nyingine

K. Walibora. “Nizikeni Papa Hapa”

4. (a) “Isije ikawa hapa habari ya kufuata asali ukafa mzingani.” “… Pana hasara gani nzi kufia kidondani?”

(i) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 5)

(ii) Andika mbinu mbili za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 2)

(b) Hadithi, Nizikeni Papa Hapa inahimiza uwajibikaji. Jadili.(alama 5)

5. (a) Onyesha jinsi unafiki unavyoshughulikiwa katika hadithi, “Shogake Dada ana Ndevu.” (alama 8)

(b) Changanua mtindo katika dondoo lifuatalo: (alama 12)

“Bi. Hamida alitunga donge kifuani mwake. Na donge likaja juu. Likampanda na kumsakama kooni. Kweli? Uongo? Kweli au uongo yale maneno ya binti yake?

Labda kweli anamfıkiria mambo mabaya binti yake tu. Labda kweli dhana yake ni mbovu. Bi. Hamida alichanganyikiwa na mambo.

Alivutwa huku na huku na nafsi yake yenye chagizo. Upande mmoja sauti yake ya ndani ilikuwa inamtetea Safia, na upande wa pili wa nafsi yake ilikuwa ikimshuku Safia; na sauti zake zote mbili hizo zimo ndani ya kiwiliwili chake zinamvuta yeye mtu mmoja, Bi. Hamida. Hatimaye hakutambua afanye nini.”

SEHEMU D: USHAIRI

Jibu swali la 6 au la 7.

6.Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

Lilipo lile banda, lile pale,
Kuna tuja kakonda, kwa uwele,
Wala siye kupenda, hiyo ndwele,
Ndwele ya kutishwa!

Ni ndwele ya kutengwa, penye haki,
Uwele wa kusutwa, pasi haki,
Ugonjwa kupuuzwa, na miliki,
Ndwele ya kutwishwa!

Mwiliwe kawa sugu,
viwandani, Uso una kunyugu,
ziso fani, Ujira wake ndugu,
ni mapeni, Ndwele ya kutwishwa!
Na homa akipatwa, maishani,
Kwa tiba apuuzwa, kama nyani,
Hajulikani kuwa, yeye nani,
Ndwele ya kutwishwa!

Ana chawa nyweleni, ona dhiki,
Na kunguni nguoni, ahiliki,
Funza na miguuni, wamesaki,
Ndwele ya kutwishwa!

Bado yuasubiri, kisimati, Dhiki yake kutiri, ‘we tamati Ndipo iwe sururi, ya kidhati Nyota yake ni nyota ya huzuni.

(K.Wamitila)

(a) Fafanua kwa kutoa hoja sita kutoka kwenye shairi, jinsi nyota ya anayerejele wa ni ya huzuni. (alama 6)

(b) Eleza muundo wa shairi hili. (alama 6)

(c) Bainisha aina zifuatazo za uhuru wa kishairi katika shairi: (alama 6)

(i) inkisari

(ii) kujifanyanga sarufi

(d) Eleza tamthali tutu za usemi zilizotumiwa katika shairi hili. (alama 3)

(f) Eleza sifa mbili za anayelengwa katika shairi hili kwa kurejelea ubeti wa mwisho. (alama 2)

(g) Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (alama 2)

7. Soma Shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.

Kalma akili si mali, maskini na tajiri
Wangalimoja sampuli, asikuwepo fakiri
Na hangekuwa na mali, mwinyi bila kufikiri
Kama akİlİ si mali, usingeweza fikiri.

Ukeshapo kwa fikara, ni kwa wingi wa akili
Kuwaza kigaragara, una mengi si kalili
Na kuwa una tambara, metajirika kwa hili
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.
Alokijenga kitanda, ana wingi wa akili
Hata asiwe na bunda, hamithili kwa akili
Hata naye paka nunda, pasipo akili hali
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

Akili kweli ni mali, kwa kuteua vya mwozo
Singetumia akili, ungevila vya angamizo
Afya ikawa thakili, na kuhiliki mawazo
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

Vipi gonjwa kikuganda, wawazia spitali?
Huachi ukawa ng’onda, ukanyauka muwili
Ugangani unakwenda, kutafuta afadhali,
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

Kama akili si mali, kusingekuwa na jela,
Kuwatenga kuwa mbali, wenye hiana na hila,
Kwa mbavu na ufidhuli, pamwe mbinu tolatola,
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

Tajiri na maskini wote wanayo akili,
Ni kuwa hayafanani, waliyonayo makali
Kabisa hawashibani, liwe lile au hili,
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

Kalma akili si mali, ‘singekuwa na hazina
Ya kudadisi mithali, na kumpinga yako mnna
Gani inadumu mali, kuliko huko kusana?
Kama akili si mali, usingeweza fikiri.

(T. Arege)

(a) “Ufanisi wa binadamu hutegemea akili.” Fafanua kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye shairi hili. (alama 6)

(b) Andika mifano ya vipengele vifuatavyo vya kimtindo katika shairi hili:(alama 4)

(i) sitiari

(ii) tanakuzi

(iii) Swali la balagha

(iv) kinaya

(c) Eleza mbinu nne ambazo mshairi ametumia kutosheleza mahitaji ya kiarudhi. (alama 4)

(d) Andika aina mbili za urudiaji zinazojitokeza katika shairi hili.(alama 2)

(e) Fafanua muundo wa shairi hili.(alama 4)

SEHEMU E: FASIHI SIMULIZI

8. Soma utungo ufuatao kisha ujibu maswali. Shangazi anambila
umewadia muda
wa kukiacha kiambo
cha Baba
Nende kujinasibisha
na ajinabi tusohusiana
kwa ngeu wala usaha
nache niwapendao
nache aila
nache matamanio
ya elimu kufuatiya.

Anambile shangazi
Hino ni neema
ela moyo wanirai
“Wajitia shemere”, nami nauambia,
“Najua si utashi wangu”
ila hiari sina

kwani lvii ni faradhi
mitamba mepokelewa
na ami kwa furaha
kilobaki ni kuvuka
kizingiti hiki.”
Kwaheri’i Mama, kwaheri wanuna.

(a) Ainisha wimbo huu kwa kuzingatia kipengele cha maudhui.(alama 2)

(b) Andika sifa mbili za jamii inayosawiriwa na wimbo huu. (alama 2)

(d) Unanuia kutumia mahojiano kukusanya habari kuhusu nyimbo za aina hii.

(i) Eleza manufaa matano ya kutumia mbinu hii.(alama 5)

(ii) Eleza changamoto tano za kutumia mbinu hii.(alama 5)

Kiswahili Karatasi 3 (102/3)

MAJIBU

1. Haya ni maneno ya Msimulizi/mwandishi

Yanamhusu Selume

Selume yumo kwenye kituo cha Afya cha Mwanzo Mpya/ yanarejelea mandhari/ mazingira ya Kituo cha Afya cha Mwanzo Mpya

Anawazia changamoto alizopata alipokuwa akifanya kazi kwenye hospitali ya umma. Kwa mfano, ukosefu wa vifaa vya kimsingi kama vile glavu.

Hali imekuwa afadhali baada ya kuajiriwa katika kituo cha Mwanzo Mpya. 4x 1 = (alama 4)

Tanbihi

a. Dondoo limetolewa uk. 140.

b. Mtahiniwa atuzwe kulingana na hoja anazotolea jibu sahihi.

Hata akikosea msemaji, atuzwe kwa Yale mengine.

ii

(i) Nahau — ameyapa kisogo

(ii) Tashbihi — kama mana iliyomdondokea kinywani

(iii) Istiari – mana 2 x 1 = (alama 2)

Selume anaonyesha athari za tofauti za kisias a. Anafarakana na mume wake kwa sababu alimuunga mkono Mwekevu uk. 30.

Mwandishi amemtumia kuendeleza maudhui ya ukabila. Mume wake anaoa msichana wa kikwao (uk. 35) baada ya kufarakana.

Ametumiwa kuonyesha tabia za wahusika wengine. Kupitia kwake tunaona utu wa Ridhaa. Ridhaa anamtuliza na kumtafutia kazi (uk. 35)

Ni kielelezo cha udugu wa wanyonge. Yeye na wenzake wanamsaidia Ridhaa kukabiliana na hali ya ukiwa iliyosababishwa na kufiwa na familia yake. Anachimuza changamoto/uovu uliopo katika taasisi za umma. Analalamikia ukosefu wa vifaa vya kimsingi kama vile glavu. Analalamikia ukosefu wa huduma muhimu kama vile umeme, kuuzwa kwa dawa zilizotengewa wanyonge…. (uk. 140)

Kupitia kwake tunaona jinsi kuzingatia tamaduni bila tahadhari kunaweza kuleta maangamizi. Anamwelekeza Tuama awashauri wenzake dhidi ya kupashwa tohara/ kufuata mila bila tahadhari (uk. 143)

Anaendeleza ploti. Ndiye anayehadithia kisa cha Kipanga ambaye alianza kutumia pombe vibaya kwa kukataliwa na aliyemdhania kuwa babake (uk. 143)

Kupitia kwake mwandishi anaonyesha umuhimu wa mshikamano wa kifamilia katika maadili ya wana. Kukataliwa na baba kunamfanya Kipanga kuwa mraibu wa pombe. Ni kielelezo cha wanaowajibika kazini- anawahudumia wagonjwa.

6x 1= (alama 6)

(I) Chandachema

(i) Kumwaga dukuduku -kuwasimulia wenzake kisa chake ili kupunguza mwemeo wa matatizo yake. Anawasimulia Umulkheri, Zohali, Mwanaheri na Kairu kisa chake. (uk. 102)

(ii) Kujitenga na mazingira- Anaondoka kwa jirani baada ya Satua- mke wa jirani kuanza kumwona kama mzigo (uk. 103). Anaondoka kwa Tenge anapoona mazingira hayo hayamridhishi/ ya upujufu wa maadili.

(iii) Kuwasaka walezi/kutaka kurudiana na walezi/ukoo. Chandachema anatafuta asili ya mama yake, Rehema. Anapobaini ameolewa anahiari kutoendelea kumtafuta, (Uk. 104)

(iv) Kufanya maamuzi/kuchukua msimamo imara wa kujitegemea. Chandachema anasema kwamba hataenda kwa shangazi yake kulelewa huko; haihalisi kumwongezea mzigo (uk. 104)

kwani ndiye aliyekuwa akigharamia masomo yake tangu hapo.

(v) Kujiendeleza kielimu/ kuamua kutumia uwezo wao katika elimu kujiendeleza.

Anaamua kuenda katika shamba la shirika la chai( la Tengenea) kwani alijua pana shule hapo; ataweza kujiendeleza kielimu (uk. 105).

(vi) Kutafuta ajira. Chandachema anapoona hawezi kuishi /kujiendeleza kiuchumi katika mazingira ya nyumbani mwa Bwana Tenge, alianza kuchuma majani chai kwa malipo kidogo akiwa darasa la tano. (uk. 106)

(vii) Kuweka siri/kutosema kuhusu maamuzi yao iii yasivurugike. Chandachema hawaambii walimu wake kwamba amehama kwa BwanaTenge hadi anapofanya mtihani wake. (Uk. 107)

(vii) Kutia bidi masomoni- Anasema atajitahidi masomoni (uk, 108) . Anafanya vyema katika mtihani wake. 4 x 1 = (alama 4)

(ii) Dick

(i) Anaingilia ulanguzi wa dawa za kulevya kwa kuhofia adhabu ya mwajiri wake.

(ii) Kutaka kukidhi mahitaji ya kimsingi kunamsukuma kuingilia ulanguzi wa dawa (uk. 122)

(iii) Kuuona/kuichukulia hatua/kuuchukulia uamuzi anaotoa kuhusu kuingilia uovu kama majaliwa hivyo kupunguza uzito wake. Anasema ulanguzi ndio hali aliyoandikiwa na Mungu (uk. 122 — 123).

(iv) Anatathmini matendo yake na kuwazia athari za matendo hayo. Anaamua kuacha ulanguzi wa dawa(uk. 134).

(v) Kujiendeleza kitaaluma. Anasomea Teknolojia ya Mwasiliano baada ya kupokea nasaha kutoka kwa Mwangeka, kwa njia hii anakinga dhidi ya kurudia mazoea yake ya awali. (uk. 174)

(vi) Ujasiriamali; Anaanzisha biashara ya vifaa vya mawasiliano ambayo inamwezesha kujitegemea na kuwaajiri wenzake; (uk. 174) 4x 1 = (alama 4)

2. (a) (I) Tunu na Sudi kujitolea kuwa na mfumo wa kuongoza harakati za ukombozi/kupiga vita

udhalimu. Kwa mfano walikuwa watetezi wa haki hata wakiwa wanafunzi chuoni.

(ii) Sudi kukataa ushawishi wa viongozi dhalimu. Anakataa kuchonga kinyago cha Majoka

hata baada ya kushawishiwa na Kenga (uk. 11-12)

(iii) Sudi kuwatia hofu viongozi dhalimu kwamba matendo yao yanamulikwa na washikadau

kama vile Jumuiya ya Kimataifa (uk. 12)

(iv) Kuwazindua wanyonge kuhusu hila za viongozi. Sudi anadhamiria kuwazindua Kombe

na Boza. (uk. 14)

(v) Kuchunguza mienendo ya viongozi dhalimu. Ashua na Tunu wanatambua kwamba kuna

mkutano wa Kenga na kutaka kujua wanachopanga. (uk. 15)

(vi) Kuwaita/kuwakusanya na kuwaongoza warn wasikilize na kukabili viongozi dhalimu. (uk. 15)

(vii) Migomo ya wauguzi na walimu kudai haki zao (uk. 16)

(viii) Kuwakabili viongozi dhalimu moja kwa moja na kuwaambia makosa yao.

Ashua anamkumbusha Majoka kuwa hakuna mchuuzi asiyelipa kodi na kuwa hela hizo zingesafisha soko (uk. 25)

(ix) Maandamano — Tunu pamoj a na wanaharakati wanaongoza maandamano kwa madhumuni ya kutetea haki za Wanasagamoyo na kupinga utawala dhalimu (uk. 32)

(x) Mikutano ya hadhara na ya wachache, kwa mfano, hotuba ya Tunu kwa wanahabari iliyoangazia ukiukaji wa haki za Wanasagamoyo (uk. 32)

(xi) Kuamua kuunga mkono uongozi ufaao bila kuzingatia tabaka, jinsia au umri.

Raia wanamteua/wanamuunga mkono Tunu, Sudi kukataa kuchonga kinyago cha Majoka na kuchonga cha Tunu. (uk. 19)

(xii) Tunu alisomea uanasheria kwa madhumuni ya kupigania haki za Wanasagamoyo.

(xiii) Ashua kukataa ajira katika shule ya Majoka.

(xiv) Baadhi ya Wanasagamoyo kuususia mkutano wa Majoka.

(xv) Matumizi ya vyombo vya habari kama vile Runinga ya Mzalendo kuihamasisha umma.

(xvi) Upelelezi wa nje kuchunguza kifo cha Jabali.

(xvii) Ufadhili wa nje kwa wapigania haki za Wanasagamoyo. Hoja 10 x 1 =( alama 10)

b) i) Maudhui

(I) kumbukumbu kuhusu mauaji ya Jabali inaonyesha ukatili (uk. 34).

(ii) Tunarudishwa nyuma kuonyeshwa Sudi na Tunu walipoanza harakati za utetezi wa haki walipokuwa chuoni. (uk. 18)- Maudhui ya utetezi wa haki yanajitokeza hapa.

(iii) Kumbukizi kuhusu mashujaa kupitia tangazo kwenye redio (uk. 4) inaonyesha matumizi ya mbinu hasi za kitawala- propaganda.

(iv) Mapenzi — Ashua na Majoka walivyopendana kabla ya Ashua kuolewa na Sudi (uk. 19, 23, 49)

(v) Kumbukizi kuhusu Ashua alipofuzu na kukataa ajira katika Majoka and Majoka Academy. Mudhui yafuatayo yanajitokeza

• Utetezi wa haki

• Uzalendo

(vi) Majoka kuhadithia kuhusu ndoa yake na Husda. (uk75)Maudhui yafuatayo yanajitokeza

• Utamaduni

• Usaliti

• Uwajibikaji Hoja 5 x 1 = (Alama 5)

ii Wahusika

(i) Kutokata tamaa kwa Asiya na Ngurumo wanapomwandama Bi. Husda hadi akawapa kandarasi .

(ii) Ukatili wa Majoka- tunapoelezwa na Siti kuwa amewaua vijana wengine watano (uk. 16)

(iii) Msimamo mkali wa Tunu na Sudi katika kutetea haki za wanasagamoyo kiasi cha lona kiapo. (uk. 18)

(iv) Tabia ya Majoka ya kuling’anga’ania/kulishikilia jamb°. (uk. 20) kwa mfano, anapomkanya Ashua asimwite mzee (uk. 20)

(v) Tamaa ya Majoka —maelezo ya mzee Kenga kupitia kwa sauti yake inayompitikia Majoka mawazoni (uk. 29)

(vi) Ashua ni Msomi, kupitia kwa maneno ya Majoka anapomkumbusha kuwa ana shahada ya ualimu. (uk. 25)

(vii) Tabia ya Majoka ya dharau- kumbukizi za Majoka kuhusu kisomo cha Tunu (uk. 32)

(viii) Kuonyesha unafiki wa Majoka. Anaishi na mtu asiyempenda kupitia kumbukumbu ya Majoka (uk. 75). Hoja 5 x 1= (alama 5)

Tanbihi

i. Mtahiniwa anaweza kuanza kwa mbinu rejeshi kisha akadondoa maudhui au ukuzaji wa wahusika kutokana na mbinu rejeshi.

ii. Kutaja maudhui/ mbinu rejeshi ambapo maudhui yanapatikana.

3. i

(1) Msemaji ni Ashua

(ii) Anamwambia Majoka

(iii) Wamo ofisini mwa Majoka

(iv) Majoka anakana kwamba kuna ushahidi wa wanafunzi kugeuka kuwa makabeji kwa kudungana sumu ya nyoka/dawa za kulevya ndipo Ashua anasema haya. 4 x 1= (alama 4)

(Dondoo limetolewa uk. 26)

i. Sitiari — kipanga – kuku

Imetumiwa kuonyesha uwezo wa mwenye mamlaka juu ya mnyonge.

ii. Swali la balagha Ushahidi utatoka wapi kama kipanga ndiye hakimu kwenye kesi ya kuku?

Imetumiwa kumsuta mwenye mamlaka.

iii. Uhaishaji/ Tashihisi/ Uhuishi

Kipanga kupewa uwezo wa kuwa mtaalamu wa sheria/hakimu. Kuonyesha upendeleo wa wenye nguvu dhidi ya wanyonge.

iv Kejeli/ stihizai- kupitia kwa toni inayojitokeza.

2 x 2 = (alama 4) Kutaja 1

Dhima 1

b) (i) Mkarimu — anawaletea akina Sudi, Kombe na Boza chai na mahamri (uk. 2)

(ii) Jasiri — Anamkabili Majoka na kumwambia udhaifu wa shule yake (uk. 25-26)

(iii) Mwenye kujitunza — Anaiheshimu ndoa yake ndiposa anakataa ushawishi wa Majoka. Anamwambia, “Mimi ni mke wa mtu…”

(iv) Mwenye hasira —Anamkanya Majoka kwa ukali anapomsimanga mumewe (uk. 24)

(v) Mwenye matumaini — Ana imani kuwa maisha yatabadilika na kuwa bora soko likifunguliwa (uk. 25)

(vi) Mdadisi — Anamhoji Majoka kuhusu sababu ya soko kufungwa milele

(vii) Mwenye mdomo mchafulmpyaro. Anamwambia Sudi kuwa amechoka kupendwa kimaskini (uk. 47)

(viii) Kigeugeu — kuomba pesa kwa Majoka na hali anakashifu shule na kampuni yake, kumgeuka mumewe na kumshtumu kwa kutopata matunzo kwake.

Hoja 6 x 1 (alama 6)

(i) Kuelewa wakati wa kutukia kwa matendo kama vile maelezo kuhusu matukio nyumbani kwa kina Tunu saa mbili asubuhi.(uk. 51)

(ii) Mandhari hutambulisha/hubainisha wahusika katika onyesho (uk. 88). Tunatambulishwa kwa walinzi wa Majoka.

(iii) Mandhari yanadokeza/huonyesha hali ya mchezo kama vile mgogoro (uk. 88). Afisini mwa Majoka akiwa na Ashua, Husda na Majoka kunachimuzwa mgogoro kati ya Husda na Ashua.

(iv) Kuonyesha matatizo ya kijamii. Kwa Mamamapima tunaonyesha matumizi mabaya ya vileo. Maudhui ya ufisadi yanajitokeza

(v) Kulinganua hali za matabaka kwa mfano, Majoka na mkewe Husda wanaishi kifahari ilhali Sudi na wenzake wanafanya kazi kwenye mazingira machafu.

(vi) Kuonyesha/kueleza mahali pa tukio mchezoni, kwa mfano kwenye karakana ya kina Sudi.

(vii) Kujenga/kuibua taharuki hivyo kuendeleza msuko. Kwa mfano kwenye ambalanzi Majoka anapopepelekwa hospitali

(vii) Kubainisha/kuonyesha maudhui kama vile uozo sokoni (uk. 1)

Tanbihi

Mtahiniwa akikita hoja zake kwenye mandhari moja to kama vile afisini mwa Majoka atuzwe mradi ametosheleza hoja. Hoja 3 x 2 (alama 6)

(i) Kauli ya kwanza ni ya rafiki ya Otii.

(ii) Kauli ya pili ni ya Otii

(iii) Otii anayakumbuka mazungumzo haya. Rafiki yake alikuwa akimwonya dhidi ya wasichana Mombasa.

(iv) Anayakumbuka haya akiwa mgonjwa baada ya jamaa kuamua kuchangisha pesa za kumzikia, japo hajafa bado.

(v) Yumo kibandani mwake

Hoja 5×1= (alama 5)

Dondoo limetolewa uk. 100

(1) Kinaya — Kufuata asali ukafa mzingani

(ii) Sitiari — Kufia mzingani

– Nzi kufia kidondani

Kumaanisha kudhurika na jambo ambalo pia lina faida.

(iii) Swali la balagha — pana hasara gani nzi kufia kidondani?

(iv) Tasfida-kufuata asali

(v) Toni kali ya kusuta- isije ikawa mambo ya kufuata asali ukafa mzingani 2 x 1 (alama 2)

(i) Jamaa waneona Otii ni mgonjwa mahututi. Wanaanza kuchangisha pesa za mazishi

(lifRafiki ya Otfi anamwonya dhidi ya mahusiano ya kiholela na wasichana

(iii) Otii kutoyawajibikia maisha yake, anasema nzi kufa kidondani si hasara

(iv) Rehema kuondoka bila kumjuza Otii

(v) Jamaa kutozingatia ombi la Otii kuwa wamzike papo hapo; wanaishia kufa kwenye ajali.

(vi) Jamaa wanamsema Otii akiwa papo hapo bila kujali kuwa wanamuumiza kisaikolojia

(vii) Jamaa kushikilia mila kiasi cha kujutia baada ya ajali.

(viii) Mchezaji mwenzake Otii anamuumiza mchezoni kwa uchezaji hatari.

(ix) Maafisa wa michezo wanamtelekeza Otii baada ya kuumia

(x) Otii anapopata nafuu baada ya kuumia harudi uwanjani anaanza kufanya kazi duni bandarini ambayo ametosheka kwayo.

(xi) Kauli ya waziri wa michezo kwamba pengo aliloacha Otii halingeweza kuzibika laonyesha ukosefu wa uwajibikaji kwani hakuna aliyemjali hata pale alipoumia akiwa michezoni. (xii)Otii anawajibikia kuchezea timu ya Taifa. 6 x 1 = (Alama 6)

Tanbihi

Mtahiniwa anaweza kuonyesha uwajibikaji au kutowajibika.

c)

(i) Dennis anasoma kwa taabu.

(ii) Wazazi wa Dennis kudharauliwa na kila mtu kwa umaskini.

(iii) Wazazi wa Dennis kufanya kazi duni — vibarua vya kuwalimia matajiri mashamba.

(iv) Kutojitosheleza kwa chakula. Dennis kunywa uji chuoni kwa kukosa unga.

(v) Malazi duni. Shuka za Dennis zimechanika.

(vi) Dennis hana pesa wala hana wa kumwazima.

(vii) Dennis hana pesa za kununulia mahitaji madogo madogo (Uk. 17).

(viii) Umaskini — Dennis anakosa mahitaji ya kimsingi kama vile chakula na mavazi. Hali hii inamfanya kuogopa kutangamana na wenzake chuoni. Anapobishiwa anaogopa kuufungua mlango.

(ix) Dennis anaogopa kuhusiana kimapenzi na Penina kwa sababu ya umaskini uliomwandama.

(x) Penina anamkandamiza/anamtusi/anamdharau Dennis kwa sababu ya umaskini.

(xi) Chumba cha Dennis ni kikavu hakina chochote cha kutamaniwa.

(xii) Dennis hawezi kuzichapisha hadithi zake kwa sababu ya kukosa hela.

(xiii) Dennis anafukuzwa na Penina kwa sababu hawezi kujikimu na kumkimu yeye.

(xiv) Dennis ni mtegemezi wa wazazi wa Penina; ndio wanaowakimu kwa yote.

(xv) Anapofukuzwa anabeba chote anachomiliki kwa begi moja tu.

(xvi) Umaskini unamfanya Dennis kujutia masomo yake ambayo hayamwezeshi kujinyanyua kiuchumi. 7×1= (alama 7)

5. (a) Unafiki

(i) Safia anaaminiwa na wazazi wake ilihali anawahadaa kupitia kwa matendo yake.

(ii) Safia alimleta Kimwana wazazi wake wakijua kuwa ni msichana ilihali alikuwa mwanamume.

(iii) Anamleta rafiki yake akisingizia kuwa wanasoma ilihali wanashiriki mapenzi

(iv) Safia hujifunika gubigubi akiwa mbele ya wazazi wake ilihali alifanya kinyume akiwa faraghani.

(v) Alipoulizwa na mamake kuhusu Kali yake anasingizia kuwa ni malaria.

(vi) Kimwana huwaamkua wazazi wa Safia kwa heshima ilihali ni mtovu wa maadili¬anashiriki mapenzi na Safia.

(vii) Kimwana anajifunika sura asionekane na wazazi wa Safia waliodhani ni msichana ilihali alikuwa mwanamume.

(viii) Wazazi wa Safia wanasawiriwa kama wacha Mungu ilihali waliwasimanga watoto wa wengine.

(ix) Safia anajitetea na kusema kuwa mamake alimfikiria vibaya na kuwa yeye anajilinda.

8 x 1= (alama 8)

(b) (i) Matumizi ya nahau- alitunga donge kifuani mwake — kuonyesha uchungu moyoni

(ii) Tashhisi – donge likaja juu likampanda — kuonyesha athari za hisia/kupandwa na uchungu.

(iii) Taswira(uoni) — donge likaja juu- kuonyesha uchungu/ kujenga toni

(iv) Swali la balagha — kweli? Uongo?

Kuonyehsa mgogoro/ukinzani wa nafsi

(v) Urudiaji -kweli uongo/kweli/uongo – takriri neno- kuonyehsa mvutano akilini mwake.

(vi) Usambamba- labda kweli anamfikiria mambo mabaya binti yake; labda kweli dhana yake… kuonyesha mvutano wa mawazo

(vii) Ulinganuzi wa ukinzani wa mawazo — kumtetea/kumshuku- kuonysha hali ya shaka aliyo nayo/ kutokuwa na hakika

(viii) Tanakuzi — kweli — uongo

Kutetea – kushuku.

(ix) Chuku — sauti kumtetea — haiwezekani- kuonyesha hali ya kutoamini/ kuonyesha mwemeo wa hisia. 1 x 2 = (alama 12)

6. (a) i. Amedhoofika/amekonda kwa ugonjwa na kuteswa

i. Kudhulumiwa haki/kutengwa penye haki

ii. Kulaumiwa bila sababu.

iii. Kutofaidika kwa rasilimali/ kupuuzwa na miliki/kutothaminiwa.

iv. Kufanya kazi ngumu viwandani na kupokea ujira mdogo.

v. Kutopewa huduma za afya.

vi. Kutelekezwa katika hali duni ya maisha : chawa, kunguni; funza 6 x 1 = (alama 6 )

b)

(i) Mishororo minne katika kila ubeti

(ii) Vipande viwili katika kila mshororo isipokuwa mshororo wa mwisho

(iii) Kipande cha kwanza cha mshororo kina mizani nyingi kuliko cha pili (7,4)

(iv) Mstari wa mwisho una mizani chache (ni mfupi) isipokuwa katika ubeti wa mwisho una (mizani 11)

(v) Kila ubeti unajitegemea kivina, vina vya ndani ni tofauti kutoka ubeti mmoja hadi mwingine. Vina vya mwisho pia ni tofauti kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.

(vi) Shairi lina beti sita.

(vii) Lina kibwagizo isipokuwa ubeti wa sita. 4 x 1 = (alama 4)

(c)

(i) kawa ukawa

mwiliwe – mwili wake

ziso – zisizo

we – iwe

(ii) Kufinyanga sarufi

Na homa akipatwa — akipatwa na homa Kwa tiba apuuzwa — apuuzwa kwa tiba Funza na miguuni — na funza miguuni 2 x 1 = (alama 2)

(d) (I) Tashbihi kama nyani

(ii) Kinaya kufanya kazi ngumu kwa malipo duni

(iii) Sitiari – ndwele – matatizo

– Nyota – bahati/mustakabali 3 x 1= (alama 3)

(e) Mtetezi wa haki / mzindushi 1 x 1 =(alama 1)

(f) (i) mwenye tumaini – bado yuasubiri

(ii) Ana bahati mbaya – Nyota yake ni nyota ya huzuni 2×1=(alama 2)

(g) Anapopatwa na homa/anapokuwa mgonjwa yeye hupuuzwa kama nyani. Hakuna anayemtambua; hayo ni matatizo ya kusababishiwa/ ni ugonjwa wa kusababishiwa. 4 x 1/2 = (alama 2 )

7. (a) i) Kama watu wasingekuwa na akili watu wote wangekuwa sawa; matajiri na maskini/ Akili humwezesha mtu kuwa tajiri/mwinyi.

(ii) Akili humwezesha mtu kuwazia hall yake;

(iii) Humwezesha kuunda vifaa vya kuyarahisisha maisha-kuunda kitanda.

(iv) Humwezesha kupata chakula- bila akili hata nunda hapati chakula.

(v) Akili humwezesha mtu kubagua vilivyo vibaya; hadhuriki, hivyo kusetiri afya yake.

(vi) Humwezesha mtu kupata matibabu kwa ndwele; anawazia spitali.

(vii) Akili huwezesha kutenga wahalifu na wasio wahalifu.

(viii) Humwezesha binadamu kuweka akiba; humwezesha kulinda mali. 6 x 1= (alama 6)

(b) (i) Sitiari – akili si mali

– akili ni mali

– ukawa ng’onda

(ii) Tanakuzi — maskini na tajiri

(iii) Swali la balagha — vipi gonjwa kikuganda wawazia spitali?

(iv) Kinaya — kuwa na matambara na kuambiwa umetajirika kwa hili. 4 x 1 = (alama 4)

(c) (1) Inkisari — kigaragara — ukigaragara

– metajirika — umetajirika

– alokijenga — aliyekijenga (kutosheleza idadi ya mizani)

(ii) Mazida — muwili — mwili

(kutosheleza idadi ya mizani)

(iii) Udondoshaji wa maneno.

Pamwe mbinu — pamwe na mbinu (Kutosheleza idadi ya mizani).

(iv) Kufinyanga sarufi — gani inadumu mali-Mali gani inadumu

(Kuleta urari wa vina) 4 x 1 = (alama 4)

(d) i Urudiaji wa virai — kama akili si mali.

ii Urudiaji wa silabi/sauti- silabi li na ri katika ubeti wa kwanza.

iii Urudiaji wa mshororo / usambamba— kama akili si mali 2 x 1 = (alama 2)

(e)

(i) Mishororo minne katika kila ubeti.

(ii) Vipande viwili katika kila mshororo.

(iii) Vina vya ndani na vya nje vinabadilika kutoka ubeti hadi mwingine.

(iv) Shairi lina kibwagizo- kama akili si mali, usingeweza fikiri

(v) Kila mshororo una mizani 16 (8, 8)

(vi) Shairi lina beti nane.

4 x 1 = (alama 4)

8. (a) Wimbo wa harusi — nache aila, kujinasibisha na asiyehusiana naye kwa damn… , kutolewa kwa mahari

1 x 2= (alama 2)

ii) Ulipaji mahari -mitamba imepokelewa

iii)Shangazi na ami kuwa na nafasi katika ndoa. iv)Wanaooana hawana uhusiano wa kinasaba.

2 x 1 = (alama 2)

(c) i) Kushusha na kupandisha kidatu kulingana na hali anayotaka kuibua.

ii) Kuvaa maleba ya bibi harusi.

iii) Kuigiza baadhi ya vitendo.

iv) Kuihusisha hadhira pengine kwa uimbaji/kuimba pamoja.

v) Kuimba kwa kasi, wastani ili hadhira ipate taathira ifaayo.

vi) Kutumia ishara/miondoko ili kuonda ukinaifu.

vii) Kutumia ala zinazaoafikiana na ujumbe wa wimbo.

(d) I Manufaa ya mahojiano

(i) Ni rahisi kupata habari za kutegemewa kwa vile anakabiliana ana kwa ana na mhojiwa.

(ii) Anaweza kumfasiria anayehojiwa baadhi ya maswali.

(iii) Anaweza kuona sifa/ishara za use za wawasilishaji hivyo kukuza uelewa.

(iv) Majibu yanaweza kunakiliwa au kunaswa moja kwa moja yanapotolewa, hivyo kuhifadhika.

(v) Anaweza kubadilisha mtindo wa kuhoji kulingana na kitembo cha elimu/uelewa wa anayehojiwa.

(vi) Anaweza kung’amua wakati anapopewa habari zisizo za kweli hivyo

kutozinakili.

(vii) Kwa vile anakabiliana na mhojiwa si rahisi kwa mhojiwa kukataa kujibu maswali.

(viii) Mahojiano yanaweza kutolewa kupitia kwenye simu, hivyo kupunguza gharama. 5 x 1 =(alama 5)

II Changamoto

(i) Tatizo la kimawasiliano huenda likaathiri utoaji wa habari.

(ii) Huenda mhoji/mhojiwa asiwe na muda wa kutosha wa mahojiano.

(iii) Mhojiwa kumshuku mhoji, hivyo kutotoa habari za kutegemewa.

(iv) Mhoji kuwajaza wahojiwa hofu kutokana pengine na kiwango chake cha elimu.

(v) Kwa vile wahojiwa wanakabiliana na mhoji moja kwa moja, huenda wakampa habari za uongo ili kumfurahisha.

(vi) Ikiwa matini ya mahojiano imeandikwa kwa lugha tofauti na ajuayo mhoji, huenda pakawa na tatizo la kutafsiri.

(vii) Ni njia ghali kwani kwa kawaida mtafiti sharti asafiri kukutana na mhojiwa.

(viii) Anayehoji akishindwa kuibua maelewano baina yake na mhojiwa mwanzoni, huenda mawasiliano yakatizwe, hivyo kuathiri vibaya utoaji wa habari. 5 x 1= (alama 5)